Monday, December 24, 2012

KULIKONI PAUL SCHOLES!



Mwisho: Scholes, Giggs na Rio Kuachia ngazi
Paul Scholes
LONDON, ENGLAND
MKONGWE Paul Scholes amepanga kustaafu soka mwishoni mwa msimu huu wakati kocha wa Manchester United, Alex Ferguson akijipanga kufumua kikosi chake.

Pia maveterani wengine wa Manchester United, Ryan Giggs na Rio Ferdinand nao wako njia moja kubwaga manyanga.
Scholes amewaambia rafiki zake kuwa atastaafu soka mwezi Mei mwakani na safari hii hatabadili mawazo.

Ferguson anajiandaa kuweka mambo sawa kwenye kikosi chake kwani hata nahodha wa timu hiyo, Nemanja Vidic kwa muda mrefu sasa amekuwa anakabiliwa na tatizo la goti.

Hivi karibuni alitumia watu wake kumfuatilia beki wa Benfica, Ezequiel Garay.

Watu hao walimwangalia wakati Benfica ilipocheza dhidi ya Sporting Lisbon na Olhanense.

Pia anamfuatilia beki wa kati wa Molde na timu ya taifa ya Norway, Vegard Forren.


Garay, ambaye aliwahi kuchezea Real Madrid, amekuwa hana furaha katika kikosi hicho kutokana na klabu kushindwa kulipa mishahara yake.

Garay, ambaye amechezea timu ya Taifa ya Argentina mara 11, pia anafukuziwa na Juventus.

Scholes aliachana na soka katika msimu wa 2010-11, lakini aliamua kurudi uwanjani mwezi Januari mwaka huu.
Aliombwa na Ferguson kuendelea kucheza msimu huu na amecheza mechi 13.

Scholes anaamini kuwa umri umemtupa mkono na asingeweza kucheza soka kwa muda mrefu.
Giggs anamzidi mwaka mmoja Scholes na amecheza mara nane tu msimu huu.

Ingawa kuna taarifa kuwa Giggs bado hajafikia uamuzi wa mwisho kuhusu kuachana na soka.

"Kwa sasa nimekuwa bize nikifanya mafunzo ya ukocha, hayo mambo ya kustaafu sijafikia uamuzi wa mwisho."

Paul Scholes
Umri: 38
Mechi: 710
Mabao: 155
Alijiunga na United: Julai 8, 1991
Aliichezea mara ya kwanza: Sept 21, 1994 v Port Vale (ugenini)