Monday, May 20, 2013

Refa akitolewa damu mechi ya Simba na Yanga


Kipa wa Yanga, Bartez,akiokoa mpira wa penati kwenye pambano la soka ligi kuu Tanzania bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.


Yanga jana ilianzisha sherehe za ubingwa wake wa 23 wa ligi kuu ya Bara kwa kishindo baada ya kuwafunga mahasimu Simba 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, katika mchezo ambao mpishi wa mabao hayo alikuwa na bahati kuwa uwanjani kuyatengeneza na mwamuzi Martin Saanya kupasuliwa usoni kwa ngumi ya mchezaji na kutibiwa uwanjani akiwa amelala kwenye nyasi kwa dakika tano.
Ikiwa imebaki dakika moja mpira kumalizika, Saidi Cholo wa Simba alionekana kusukumana kiugomvi na mchezaji Juma Abdul wa Yanga hivyo muamuzi huyo kulazimika kukimbia kwenda kutuliza purukushani hiyo pembeni mwa uwanja.
Lakini badala ya kuwa jukumu la kawaida kwake, damu ilikuwa ikivuja kutoka juu ya jicho la Saanya baada ya kuwaachanisha wachezaji.
Baada ya matibabu ya dakika tano, muamuzi huyo alimaliza sekunde zilizokuwa zimebaki mchezoni bila kutoa adhabu yoyote kwa mchezaji huyo wa Simba ambaye alionekana kurusha ngumi.
Kwa ushindi huo, Yanga ambayo imetwaa kombe na zawadi ya sh.milioni 70 kutoka kwa wadhamini Vodacom imemaliza ligi kwa kujikusanyia jumla ya pointi 60, alama 15 juu ya Simba iliyoshika nafasi ya tatu nyuma ya Azam.
Kocha wa Yanga Ernie Brandts ambaye ametwaa ubingwa wa Bara katika msimu wake wa kwanza aliwashukuru mashabiki kwa kuwaunga mkono.
Mwalimu wa Simba Patrick Liewig ambaye ana nafasi ndogo ya kubaki kwenye timu hiyo, alisema goli la mapema ndilo lililowamaliza lakini wachezaji wake walijitahidi na watafanya vizuri msimu ujao.
Didier Kavumbagu aliifungia Yanga goli hilo katika dakika ya tano tu ya mchezo, huku pasi iliyozaa bao hilo ikiwa imetolewa na mchezaji angeweza kupewa kadi nyekundu mwanzoni kabisa mwa mchezo.
Mpira wa kona uliopigwa na Haruna Niyonzima kwenye eneo la hatari la Simba ulipigwa kichwa kuelekea golini na Mbuyi Twite; Kavumbagu akaucheza kwa kichwa pia ambacho kiliparaza mlingoti wa goli na kutumbukia wavuni juu ya mikono ya Juma Kaseja.
Twite alikuwa amebaki uwanjani kwa bahati, hata hivyo, baada ya rafu mbaya aliyomchezea Hamza Chanongo katika dakika ya pili kuadhibiwa kwa kadi ya njano na muamuzi.
Yanga ikitawala mchezo kwa vipindi virefu, Simba ilipata nafasi ya angalau kusawazisha bao hilo kinyume na mwenendo wa mchezo baada ya nusu saa, lakini penalti iliyopigwa na Mussa Mude ilidakwa kifundi na kipa namba mbili wa zamani wa Simba, Ali Mustafa.
Mustafa alikuwa ameshaelekea kulia wakati Mude akienda kupiga mpira huo kushoto kwake lakini akageuka haraka kabla ya kulala na kuudaka, ikichangiwa na shuti la beki huyo wa Simba kuwa dhaifu hata hivyo.
Penalti hiyo ilikuwa imetolewa na muamuzi Saanya baada ya Nadir Haroub kuwa alimkumbatia Mrisho Ngassa na kumuangusha chini kimieleka ndani ya 18.
Hamisi Kiiza aliifungia Yanga bao la pili katika dakika ya 63 kutokana na mpira mrefu wa kurusha wa Twite, ambao ulimgonga mkononi Mude kwanza kabla ya kumkuta Mganda huyo aliyeachia shuti kali lililokita nyavu za juu.
Katika mchezo ambao Yanga ilikuwa ikijaribu kulipa kisasi cha kufungwa 5-0 na Simba katika pambano kama hilo mwaka jana huku Wekundu wa Msimbazi wakiwa wameshatwaa ubingwa pia, Yanga ingeweza kupata mabao mawili zaidi kama ingekuwa na bahati zaidi.
Kavumbagu alipiga kichwa kilichogonga mwamba wa Simba na kutoka dakika saba kabla ya bao la pili, lakini mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Nizar Khalfani uligonmga mwamba na kutoka nje baada ya kumgonga Kaseja katika dakika ya 86.
Ngassa ambaye inasadikiwa kuwa ameingia mkataba wa kuichezea Yanga msimu ujao angeweza kuipatia timu yake goli mwanzoni mwa kipindi cha pili kiunyume na mwenendo wa mchezo huo ambao Yanga ilitawala kwa muda mwingi.
Lakini akiwa ameumiliki mpira ambao ulitokana na kosa la Kelvin Yondani kutaka kuwapiga chenga washambuliaji wawili wa Simba karibu na langi lake, alifumua shuti kubwa la juu.
Timu zilikuwa:
SIMBA: Juma Kaseja, SaidiCholo, Haruna Shamte, Shomari Kapombe, Mussa Mude, William Lucian, Mwinyi Kazimoto, Abdallah Seseme (Felix Sunzu dk.48), Mrisho Ngassa, Amri Kiemba (Jonas Mkude dk.76), Haruna Chanongo (Ramadhani Singano dk 75).
YANGA: Aly Mustafa, Mbuyi Twite (Juma Abdul dk.85), David Luhende, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Athumani Iddi, Simon Msuva, Frank Damayo, Didier Kavumbagu, Hamisi Kiiza (Nizar Khalfani dk.77), Haruna Niyonzima.