Wednesday, May 22, 2013

Mwana FA aamsha wanaume fistula


Nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Hamis Mwinjuma maarufu kama MwanaFA


Nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Hamis Mwinjuma maarufu kama MwanaFA ambaye ni Balozi wa Chapa Vodacom, amesema hadhi na heshima ya mwanaume katika jamii itakuwa na uzito mbele ya jamii kwa wao kuwa tayari kutafuta suluhu ya changamoto zinazoikabili jamii na wala si vinginevyo.

MwanaFA alitoa kauli hiyo mjini Dodoma wakati wa kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu fistula iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square kuelekea siku ya fistula duniani kesho. Kampeni hiyo inadhaminiwa na kampuni za Vodacom Tanzania na Vodafone ya Uingereza ikiihusisha mikoa mbalimbali.

Balozi huyo alisema ni wazi kwamba wanaume wamekuwa wamiliki wa maamuzi katika jamii huku wakitajwa kuwa nguzo ya familia lakini sifa hizo na mamlaka hayo yatakuwa na dosari kubwa iwapo hawatokuwa pia mstari wa mbele katika kuhakikisha jamii inapata suluhisho la matatizo.

MwanaFA ambaye alikuwa akielimisha wakazi wa mji wa Dodoma kuhusu fistula, alisema tatizo hilo linatibika bila ya malipo.

“Hakuna mwanamke ambaye anapata fistula bila ya mwanaume kuwa chanzo kwa kuwa sisi ndiyo tunaowapa ujauzito wake zetu, hivyo siyo vema na haki kwa mwanaume kumkimbia mkewe au kumtenga mwanamke eti tu kwa sababu mwanamke huyo ana tatizo la fistula,” alisema balozi huyo.

“Nawaomba sana wakazi wa Dodoma hasa wanaume tubadili mtazamo tulinao juu ya fistula kwa kutambua kwamba sisi ndiyo chanzo cha wanawake kupata fistula lakini zaidi ni kwamba hilo siyo tatizo kwa kuwa tatizo ni lile ambalo halina suluhisho, fistula inatibika na tena inatibika bila malipo kwa ufadhili wa Vodacom na Vodafone, nini zaidi tunachohitaji katika hili?” alihoji Mwana FA.

Alisema uamuzi alioufanya wa kukubali kutembea nchi nzima kuhamasisha kinababa kuondokana na dhana hasi juu ya fistula ikiwamo kuhusisha tatizo hilo na ushirikina au laana na hivyo kuwakimbia wake zao au kushiriki kwa namna yoyote katika kuwanyanyapaa wanawake wenye tatizo la fistula ulikuwa ni mgumu lakini alikubali kwa kuwa anaamini jamii itamuelewa.