Wednesday, May 22, 2013

‘Profesa Jay’ Achukua gwanda.


Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Haule maarufu Profesa Jay (katikati) akionyesha kadi yake ya uanachama wa CHADEMA wakati wa hafla ya kutangaza kujiunga na chama hicho mijini Dodoma jana.Kushoto ni mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi mkono wa kulia  mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika . 


Nyota wa muziki wa kizazi kipya chini, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ pamoja na rapa wa kundi la muziki wa hip hop la Mapacha, Levison Kasulwa, wamekabidhiwa rasmi kadi za kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Zoezi hilo la kukabidhiwa kadi lilifanywa na Mbunge wa Mbeya Mjini, ambaye pia ni waziri kivuli wa kambi ya upinzani bungeni, Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi kadi hiyo, Mbilinyi alisema wasanii hao wamefanya maamuzi ya busara kwani Chadema ni chama cha kutetea haki za wanyonge na wasanii kwa ujumla.

Mbilinyi alisema yeye alipofikia uamuzi wa kujiunga na chama hicho alipokewa na kupewa ushirikiano mkubwa na makamanda wote ambao si wasanii hali inayoonyesha kuwa chama hicho hakina ubaguzi kwa mtu yeyote.

“Naamini kamanda licha ya kujiunga huku lakini utaendeleza muziki, na utashirikiana kwa hali na mali kupeleka mbele gurudumu za chama na Watanzania kwa ujumla,” alisema.
Mbilinyi alisema yeye kama angeambiwa amshauri Profesa Jay angemwambia arudi nyumbani Mikumi akawatumikie wananchi.

Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika alisema yeye ni mmoja kati ya watu waliowashawishi wasanii hao wawili ambao ni Profesa Jay na Joseph Mbilinyi kujiunga na Chadema.

Mbilinyi alisema baada ya kushawishiwa ilimchukua miaka mitano kufikia maamuzi ya kuwa mwanachama wakati Profesa Jay  ilimchukua miaka 6 hadi jana alipoamua kufikia maamuzi hayo, kitendo ambacho kinaonyesha dhahiri kuwa maamuzi waliyoyafanya ni ya dhati.

“Mtu yeyote anayefanya maamuzi kwa muda mrefu anakuwa amefanya maamuzi sahihi na yenye busara na anakuwa anajiamini katika maamuzi hayo,” alisema.

Alisema kujiunga Chadema kwa msanii huyo ni mtaji wa nyongeza ambao utasaidia kutengeneza mkakati wa pamoja kwa wasanii na kusaidia kusonga mbele.

Baada ya kukabidhiwa kadi hiyo, Profesa Jay alisema atailinda kwa gharama yeyote na atakuwa tayari kushirikiana na wapiganaji wenzake ambao ni makamanda ndani ya chama hicho katika kuhakikisha Chadema inasonga mbele na kuendelea kutetea haki za Watanzania.

“Mimi Profesa Jay ni kama daraja linalowahamisha watu wa upande huu na kuwapeleka upande mwingine wa sarafu,” alisema Jay.