Monday, May 20, 2013

FM Academia wajiandaa kwa Uzinduzi


Baadhi ya wanamuziki wakiwajibika jukwaani


Baada ya kuzunguka mikoani ikitambulisha albamu mpya ya 'Chuki ya Nini', bendi ya FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma', imesema kuwa sasa inaelekeza nguvu zake kwenye maandalizi ya uzinduzi wa albamu hiyo.
Msemaji wa bendi hiyo Kelvin Mkinga alisema wanamuziki wake watatumia muda mwingi kufanya mazoezi ya kufanikisha uzinduzi huo.
"Tunataka kuzindua albamu yetu katikati ya mwaka huu, hivyo hatuna budi kuanza kujipanga mapema kwani tumeshazunguka vya kutosha mikoani tukiitambulisha albam kwa mashabiki wa muziki wa dansi," alisema.

Alisema bendi hiyo ilishakamilisha video za nyimbo nne na kwamba wanamuziki wake wanatarajia kumalizia nyingine zilizosalia kabla ya kuzindua albamu hiyo aliyodai kuwa ni kali kuliko zilizotangulia.

"Inabidi tuharakishe maandalizi ili tuweze kuzindua albamu yetu katikati ya mwaka huu kama ambavyo tumepanga, kwani awali tulipanga kuzindua mwezi Machi lakini mambo yakawa hayajaenda vizuri," alisema Mkinga.

Mkinga alizitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo kuwa ni 'Ndoa ya Kisasa', 'Otilia', 'Fataki' na 'Neema', ambazo zimekuwa zikiporomoshwa kwenye kumbi mbalimbali za burudani na kwenye vituo vya redio na televisheni.