Friday, May 24, 2013

Maimatha kusaidia wenye Fistula



Mratibu wa shindano la 'Manywele Kigoli wa Tanzania, Maimatha Jesse amesema kuwa sehemu ya fedha zitakazopatika kwenye shindano hilo atazitoa kwa ajili kusaidia wanawake wanaosumbuliwa na tatizo Fistula.
Mratibu wa shindano la 'Manywele Kigoli wa Tanzania', Maimatha Jesse
Maimatha alisema hayo wakati akizungumzia mipango inayoendelea na kufanikisha shindano hilo linalotarajiwa kufanyika Julai mwaka huu kwa kushirikisha vimwana kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

"Fistula ni miongoni mwa tatizo kwa wanawake wengi, hivyo mimi kama mratibu shindano la Manywele Kigoli wa Tanzania, nimeshauriana na wenzangu na kuamua kuwa sehemu ya mapato ya shindano yatatolewa kusaidia waathirika," alisema.

Aidha, alisema kuwa uzinduzi wa shindano hilo utafanyika Ijumaa ijayo kwa kushirikisha wasanii kadhaa wakiwamo Samir, Timbulo, kundi la Wane Star pamoja na bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo.

"Uzinduzi huo ndiyo mwanzo wa kuelekea kwenye shindano letu kwani baada ya hapo washiriki wataingia kambini kujiandaa na mchuano, ambapo tumepanga sehemu ya viingilio itatolewa kusaidia matibabu kwa wagonjwa wenye Fistula," alisema Maimatha.

Alifafanua kuwa shindano hilo litashirikisha vigoli kutoka mikoa ya Tanga, Morogoro na Dar es salaam ambao watakuwa wamepatikana baada ya kufanyika kwa usaili utakaoendeshwa mara tu baada ya uzinduzi.