Friday, May 24, 2013

Kiongozi mwingine Z'bar amwagiwa tindikali


Wimbi la viongozi wa Serikali, dini, wanasiasa na wafanyabiashara kuhujumiwa kwa ikiwamo kumwagiwa tindikali limeendelea kujitokeza Zanzibar, baada ya Sheha wa Shehia ya Tomondo, Muhamed Said ‘Kidevu; kumwagiwa tindikali nyumbani kwake mtaa wa Tomondo mjini Zanzibar.

Tukio hilo limetanguliwa na kumwagiwa tindikali Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga, aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya mji wa Zanzibar Rashid Juma, na wamiliki watatu wa maduka ya pombe wenye asili ya Kiasia na mmoja alifariki dunia.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis, alisema kwamba Sheha huyo alimwagiwa tindikali juzi usiku majira ya saa mbili za usiku, na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka na mtu aliyehusika na shambulio hilo.

Alisema kwamba Polisi baada ya kufika katika eneo la tukio walifanikiwa kuokota kopo lililokuwa na maji maji yanayosemakana kuwa tindikali na litatumika kwa shughuli za uchunguzi ikiwamo vipimo vya vidole na vipimo vyingine kwa kutumia mashine maalum ya vinasaba (DNA).

“Tumepata kikopo katika eneo la tukio, tutaangalia finger print na DNA pamoja na kutafuta walioshuhudia tukio hilo, matukio haya yanajirudia mara kwa mara, yanaweza kukomeshwa endapo wananchi watatoa ushirikiano kwa kuwataja wahusika” alisema Kamanda Mkadam.

Sheha huyo ambaye alilazwa katika hospitali ya Mnazi mmoja na kupatiwa matibabu chini ya ulinzi wa polisi, alisema baada ya kutoka msikitini alikwenda kununua chakula na kupeleka nyumbani kwake, lakini kabla ya kula chakula hicho aliamua kwenda kuchota maji nje ya nyumba yake.

Alisema akiwa amebeba ndoo mbili za maji, ghafla alikutana uso kwa uso na mtu aliyekuwa ameshika kitu mkononi na kumwagia sehemu za kichwani, usoni na kifuani na kukimbia.

“Nilipotoka kuchota maji, nilikutana na jamaa amebeba kikopo, mrefu, mweusi na amevaa ninja (mavin guy), akanimwagia kitu kama maji maji, baadae nikayahisi kuwa ni ya moto, nikapiga kelele, akakimbia na kutupa kikopo na kuanza kumfukuza, lakini nilishindwa kuendelea kutokana na maumivu makali," alisema Sheha Mohamed.

Alisema ana wasiwasi kuwa chanzo cha kumwagiwa kwake tindikali, ni kitendo chake cha kuwasindikiza Polisi katika eneo moja la mtaa wake, kuteremsha bendera mbili za Jumuiya ya Uamsho na mihadhara ya Kiislamu Zanzibar(Jumiki).

“Kwa hali hii tunayokwenda nayo Zanzibar, watatumaliza, matumizi ya tindikali yamekuwa silaha za maangamizi, tindikali imekuwa na nguvu kuliko hata silaha za moto,” alisema Sheha huyo na kuongeza.

“Kazi zetu ni za visasi, kutishiwa na kumwagiwa tindikali ni jambo la kawaida, ila ujumbe wangu kwa Watanzania siasa itatufikisha pabaya.” 

Kwa upande wake, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema Serikali itatumia nguvu zake kuwasaka watu waliohusika na shambulio hilo na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema matukio ya watu kumwagiwa tindikali yamekuwa yakijirudia na kutaka vyombo vya ulinzi na usalama, kuongeza nguvu za kukabiliana na watu wanaofanya vitendo hivyo kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.