Wednesday, May 22, 2013

Gesi Mtwara: Vipeperushi vyapingana


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa


Hali ya wasiwasi imeendelea kuwakumba wakazi wa mkoa wa Mtwara kufuatia watu wasiojulikana kuendelea kusambaza vipeperushi vya uchochezi wakishinikiza gesi isisafirishwe kwa bomba kwenda jijini Dar es Salaam, lakini wengine wakipinga ilani ya kusitisha biashara zao leo.

Moja ya kundi hilo limetuma ujumbe mfupi wa maneno kwa wananchi wa mikoa hiyo ukiwataka wasitishe shughuli zao wapate fursa ya kusikiliza hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini inayowasilishwa leo bungeni mjini Dodoma itakayowasilishwa leo.

Hii ni mara ya pili kusambazwa kwa vipeperushi hivyo. Mara ya kwanza ilikuwa Alhamisi wiki  iliyopita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa, amethibitisha kusambazwa kwa vipeperushi na ujumbe mfupi wa maneo katika simu za mikononi vilivyoonekana katika maeneo kadhaa ya Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani vikiwa na ujumbe mbalimbali.

Ujumbe mfupi uliotumwa katika simu za mikononi unaeleza kuwa “Hii ni kwa wakazi wote wanaoishi mikoa ya kusini… kuanzia vijiji na wilaya zote… tunakumbushana kuwa siku ya Jumatano tarehe 22,05,2013 kuanzi saa 3:00 asubuhi tusikilize bunge la bajeti juu ya uwasilishaji wa bajeti ya Nishati na Madini ili tujue hatima yetu wana-kusini juu ya gesi yetu.”

Umezidi kueleza kuwa: “Kama kawaida yetu siku hiyo hakutakuwa na kazi yoyote, huduma zote za kijamii zisitishwe kuanzia bodaboda, daladala hata gari za mikoani na….(onyo ukikutwa umekiuka agizo la wana-kusini kazi kwako)…tuma ujumbe huu kwa wana-kusini wote…gesi haitoki hata kwa bomba la peni.”

Hata hivyo, kundi la watu wengine wasiofahamika lilisambaza vipeperushi vya kupinga uchochezi huo ambavyo vilikuwa na ujumbe mbalimbali.

“Wana-kusini tusiwe wajinga tuamke, kweli gesi yetu ni mali yetu wote wana-kusini. Kama ni kunyanyasika serikali ya nchi yetu ilitutupa kabisa. Tarehe 17.05.2013 tuliungana kufunga maduka na biashara zote wala Shilingi hatukupata hata chakula. Je? sasa Jumatano tena tusifanye biashara. Tuacheni ujinga, wana-kusini wenzetu wengine hata kazi hawana, gesi itazidi kutufanya tuwe maskini.

Ujumbe huo unawatahadharisha wananchi hao kuwa leo wasidanganyike kwa kusitisha shughuli za uzalishaji.

Kutokana na vipeperushi na ujumbe huo, Kamanda Sinzumwa amewahakikishia wakazi wa mkoa wa Mtwara kutoogopa vitisho hivyo na kuwataka kuendelea na shughuli zao.

“Nawaombeni sana wananchi wa mkoa wetu acheni kusikiliza maneno ya watu ambao wamekuwa wakitaka kuvunja amani yetu, endeleeni na  shughuli zenu kama kawaida, msiogope vitisho, na ulinzi utaimarika kama ilivyokuwa siku ya Ijumaa ya tarehe 17,05,2013.”

Sinzumwa aliwaomba wananchi wa mkoa huo kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa mbalimbali pale watu ama kundi la watu wanapojitokeza kutaka kuvuruga amani ya mkoa huo.
Kamanda huyo aliwataka wananchi hao kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa leo Jeshi lake litaimarisha ulinzi.

Desemba mwaka jana, wakazi wa Mkoa wa Mtwara waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.

Maandamano hayo ambayo yaliwashirikisha wananchi wa wilaya za Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambalo gesi asilia inapatikana.

Waandamanaji hao walitoa maazimio kadhaa mojawapo likihoji sababu za mitambo ya kuzalisha umeme kutojengwa Mtwara ambako ni jirani na inakochimbwa gesi hiyo.

Walisema serikali haijaweka wazi namna gani wakazi wa Mtwara watanufaika na gesi hiyo wakati serikali ikiwa tayari imeshazindua ujenzi wa bomba kwenda Dar es Salaam na kutaka ujenzi huo usitishwe.

Pia alisema kuwa uamuzi wa kupeleka gesi Dar es Salaam unapingana na tamko la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa kwenye ziara yake mkoani Mtwara mwaka 2009 kwamba mkoa huo ujiandae kuwa ukanda wa viwanda.

Aidha, walitaka vinu vya kuzalishia gesi vijengwe Mtwara kwa kuwa wanayo maeneo ya kutosha ya ujenzi huo tofauti na Dar es Salaam.

Kadhalika, walisema serikali haijaeleza athari zitakazopatikana kutokana na uchimbaji wa gesi katika eneo hilo na namna itakavyoweza kusaidia kuziondoa, huku wakitaka gharama za uunganishaji wa umeme wa nyumbani zisizidi Sh 50,000 ili kila mwananchi aone ananufaika na gesi hiyo.

Maandamano hayo yaliratibiwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, TLP, APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP, yakiwa na kaulimbiu ya “gesi kwanza vyama baadaye”.å